Nitawalishaje watoto wenye umri zaidi ya miezi 6
Katika miezi 6 ya kwanza, mtoto mchanga huwa katika hatari kubwa. Kumnyonyesha humlinda kutokana na kuharisha na magonjwa mengine, na humpa mtoto muanzo mwema maishani.
Mtoto anapofikisha miezi 6, anahitaji vyakula na vinywaji vingine isipokuwa maziwa ya mama. Hivi humpa nguvu, protini, vitamini na virutubisho vingine ili aweze kukua.
Vyakula tofauti tofauti - mboga na matunda, nyama, kuku, samaki, mayai na maziwa - husaidia kumpa mtoto lishe analohitaji. Kumnyonyesha mtoto kwa muda wa hadi miaka miwili au zaidi humpa mtoto virutubisho ambavyo humlinda kutokana na magonjwa.
Ikiwa ataanza kula vyakula vigumu akiwa amechelewa, basi mtoto huyo hapati virutubisho anavyohitaji. Hii huweza kutatiza ukuaji wa mtoto. Unapoanza kumpa mtoto vyakula hivi, anza na vile vyepesi, ukiendelea hadi vile vigumu. Unapompa mtoto vyakula tofauti tofauti, atapata lishe bora.
Chakula anachopewa mtoto lazima kilingane na mahitaji yake. Mtoto anapofikisha umri wa miezi 6, mtoto anaweza kupewa vyakula vyepesi, chakula kilichopondwapondwa, supu na uji. Anapofikisha umri wa miezi 8, watoto wengi wanaweza kujilisha vyakula vidogo vidogo. Anapofikisha umri wa miezi 12, baadhi ya watoto wanaweza kula vyakula vinavyoliwa na familia nzima.
Wazazi na walinzi wengine wanatahadharishwa kuwa wasiwape watoto vyakula ambavyo vinaweza kuwanyonga kama vile njugu, zabibu, karati mbichi au vingine vinavyoweza kumsakama mtoto kooni.