Nafanya kazi mbali na nyumbani - je niendelee tu kumnyonyesha mtoto wangu

From Audiopedia
Jump to: navigation, search

Wanawake wengi siku hizi hufanya kazi mbali na nyumbani. Hii inaweza kufanya mambo kuwa magumu kwa mama kumnyonyesha mtoto wake bila kumpa chakula kingine chochote katika miezi sita ya kwanza. Lakini mtoto wako aweza kuugua iwapo hapati maziwa yako. Mama anayefanya kazi hafai kamwe kujipata katika hali inayomhitaji kuamua kati ya kazi yake na afya ya mtoto wake.

Ndiposa akina mama wanaofanya kazi wanahitaji usaidizi. Kazi zingine zinawaruhusu akina mama kuwaleta watoto wao maeneo ya kazi kwa miezi kadha. Hii inafanya shughuli ya kunyonyesha mtoto kuwa rahisi. Iwapo mama ana mtunzi karibu naye, anaweza kumnyonyesha mtoto mchana, wakati wa mapumziko. Baadhi ya waajiri hujenga vituo vya kutunza watoto wachanga ili wazazi wawe karibu na watoto wao.

Hizi ni baadhi ya mbinu za kuhakikisha mtoto wako anapata tu maziwa ya mama wakati unafanya kazi:

  • Muweke mtoto wako karibu nawe kwa miezi 6.
  • Ama kuwa na mtu atakayemleta mtoto wakati wake wa lishe.
  • Unapokuwa na mtoto mpe tu maziwa kutoka moja kwa moja kwenye titi. Iwapo unalala na mtoto usiku, huwa ananyonya sana, na hii itasaidia matiti kutengeneza maziwa zaidi.
  • Baadhi ya wanawake huomba marafiki ama jamaa, kama nyanyake mtoto, kunyonyesha mtoto wao. Iwapo unataka mwanamke mwingine kumnyonyesha mtoto wako, lazima apimwe virusi vya ukimwi na asiwe katika hatari yoyote ya kuambukizwa wakati wa kipindi chote cha kunyonyesha.
  • Njia nyingine ambayo mama anaweza kumpa mtoto maziwa yake nyakati za mchana ni iwapo atapata nafasi ya kukamua maziwa kutoka kwa matiti yake. Kisha mtu mwingine anaweza kumpa mtoto maziwa hayo kwa niaba yake. Unaweza kukamua maziwa kwa kutumia mikono mara 2 au 3 kila siku, kisha yatume ama yahifadhi ili mtu mwingine ampe mtoto wako.

MUHIMU: Maziwa ambayo hayawezi kuhifadhiwa katika mazingira baridi yataharibika na yanafaa kumwagwa yote. Iwapo maziwa yatakuwa na harufu chachu, yamwagwe. Maziwa ya mama yaliyoharibika yanaweza kumdhuru kabisa mtoto.

Sources
  • Burns, A. A., Niemann, S., Lovich, R., Maxwell, J., & Shapiro, K. (2014). Where women have no doctor: A health guide for women. Hesperian Foundation.
  • Audiopedia ID: sw010808