Jinsi ya kutumia maji ya mvua vyema katika maeneo kavu
Mbinu bora ni kupanda mazao tofauti kwa pamoja, au kupanda zao moja baada ya jingine katika shamba moja. Hii husababaisha mimea kuhifadhi maji vyema msimu wa mvua, hivyo basi kusaidia ardhi kuhifadhi maji kwa muda mrefu.
Baadhi ya wakulima huweka mifereji midogo au kingo katika mashamba yao ili kupata maji ya mvua na kuyasaidia kuloweka kwenye udongo. Hii inaitwa uvunaji wa maji. Maji ya mvua yaliyokusanywa yanaweza kutumiwa na mazao wakati wa kiangazi, na hivyo kufanya mchanga kuwa na unyevunyevu na mimea kuwa na afya hata wakati hakuna mvua nyingi.
Majira pia ni muhimu. Katika majira ya mvua panda mbegu zako mapema wakati mchanga umejaa maji.
Toa nafasi ya kutosha kati ya mimea ili kuisaidia kutumia maji vizuri zaidi haswa sehemu kavu. Katika maeneo yanayoshuhudia mvua kidogo, wakulima mara nyingi huchagua mazao yanayostahimili ukame kama vile mtama, wimbi, au mbaazi. Mazao haya yana mizizi ya kina na inaweza kuishi kwa muda mrefu bila maji. Mimea hiyo yaweza kuacha kumea wakati wa ukame na kuanza kumea tena msimu wa mvua ukirudi.
Ikiwa ardhi yako ni ngumu na imeganda kwa juu, vunja kwa utaratibu mchanga ukitumia Jembe. Hii husaidia maji ya mvua kupenyeza kwenye mchanga badala ya kutiririka.
Kwenye ardhi yenye mteremko, upandaji wa miti na nyasi kando ya kingo zake huweza kuzuia udongo kuporomoka na kupoteza maji. Panda miti na nyasi zilizo na mizizi mirefu ambayo hushikilia udongo pamoja ili kusaidia kuuweka unyevu.