Jinsi ya kulima kwa kutumia maji kidogo katika maeneo kavu
Ni muhimu sana haswa kwa wakulima kutoka maeneo kavu kutumia maji vyema. Maji yanahitajika kwa kila zao, na wakati kuna mvua kidogo, ni muhimu kutafuta njia za kuhifadhi maji kwenye mchanga kwa muda mrefu iwezekanavyo. Kwa kutumia njia zinazoweka maji kwenye mchanga, wakulima wanaweza kuendelea kulima mazao hata wakati mvua ni adimu. Wakulima wanaweza kulima chakula zaidi wakati wa ukame,iwapo watatumia mbinu za kuhifadhi maji wakati wa kupanda, kumwagilia maji kwa mimea na kutunza mchanga. Hii huboresha ardhi bora na kuhakikisha ugavi wa kutosha wa mazao. Kadiri mchanga unavyozidi kuwa bora, wakulima huona mavuno bora, hivyo basi familia na jamii kupata chakula kwa wingi. Mavuno yanapoongezeka, afya na ustawi wa jamii nzima huboreka, ikionyesha kwamba uhifadhi wa maji sio tu unasaidia kilimo lakini pia huboresha maisha kwa ujumla.
Mbinu moja nzuri ni kukuza mimea asilia ambayo kwa kawaida huhitaji maji kidogo au maji ya msimu wa mvua. Mimea hii imezoea mazingira yake na huweza kustawi kwa kumwagilia maji kidogo.
Wakulima pia wanaweza kusaidia kuhifadhi unyevu kwa mchanga kwa kutumia mbolea ya kijani na matandazo. Mbolea ya kijani inamaanisha kupanda mazao maalum ambayo huongeza rotuba ardhini na kuboresha muundo wake. Majani pia huweza kutumiwa , kwa kuenezwa juu ya mchanga ili kuuweka baridi na kuzuia maji kupotea kwa haraka.
Wakulima wanaweza pia kulinda mashamba yao yasipoteze maji kwa kujenga vizuizi. Vizuizi hivyo ni matuta madogo au mitaro ambayo hufuata sura ya asili ya ardhi. Vizuizi hivi hupunguza kasi ya maji ya mvua ili yabaki kwenye mchanga badala ya kuoshwa.