Jinsi ya kuhifadhi maji ya mvua ya kunywa
Ili maji ya mvua yawe salama kwa kunywa, ni lazima yawekwe safi , bila uchafuzi. Maji yatokayo kwenye maeneo ya barabara ya kuhifadhi maji yasitumike kwa matumizi ya nyumbani kwa sababu huwa na kinyesi na uchafuzi mwingine, maji ya barabara za lami huwa na kemikali za lami ambayo ni hatari kwa afya ya watu. Maji ya matumizi ya nyumbani yanapaswa kukusanywa kutoka kwa paa, miamba au kuchotwa kutoka kwa maji ya chini ya ardhi kwa njia ya visima vilivyochimbwa kwa mikono au visima vilivyochimbwa kutumia mashine.
Kabla ya msimu wa mvua kuanza, hakikisha umesafisha vyema tanki, bomba la kuingiza maji, paa na mifereji ya paa. Hii itaondoa uchafu au mkusanyiko wowote ambao unaweza kuathiri ubora wa maji. Pia ni muhimu sana kuepuka kutumia mitungi ambayo imewahi kuhifadhi vitu vyenye madhara kama vile mafuta, dawa za kuulia wadudu, au kemikali zozote zenye sumu, kwani hizi zinaweza kufanya maji kutokuwa salama kunywa.
Mvua ya kwanza ya mwaka inapokuja, wacha ioshe kwenye tanki ili kulisafisha. Kusunza tanki kwanza husaidia kuondoa vumbi au uchafu uliobaki. Baada ya hayo, funika tanki na uweke kichungi au skrini juu ya viingilio ambapo maji hutiririka. Hii huzuia wadudu, majani, na uchafu mwingine, pia huzuia mbu kuzaana ndani ya maji.
Kwa maji safi zaidi, ni bora kuyatoa kupitia mfereji ikiwezekana. Hii huzuia chombo kuzama ndani ya maji, ambapo inaweza kuchafua tangi. Ikiwa utahitaji kutumia ndoo au chombo kingine kuchota maji, hakikisha chombo hicho ni safi kila wakati. Hii itapunguza hatari ya vijidudu au uchafu kuingia ndani ya maji.
Kwa usalama zaidi, unaweza kutumia kichujio cha maji kinachounganisha moja kwa moja kwenye tanki. Hii itasaidia pia kutokoroga au kusogeza maji kwenye tangi. Kwa njia hii, uchafu wowote au vijidudu ambavyo vinaweza kuwa vimeingia vitatua chini.
Pia, kumbuka kufagia paa mara kwa mara ili kuzuia uchafu kuenda kwenye tangi wakati wa mvua. Ukifuata hatua hizi utasaidia kuweka maji yako ya mvua salama na safi kwa kunywa na matumizi mengine.