Jinsi ya kuchagua mfumo sahihi wa unyunyizaji maji
Mifumo ya gharama kubwa ya unyunyizaji maji hutumika katika kilimo cha kiufundi na cha viwandani. Mifumo hiyo huwa ghali sana. Hata hivyo, mkulima wa mazao kidogo anaweza kununua na kuanzisha mfumo wa unyunyizaji maji. Ikiwa itatumika kwa kukuza mazao ya soko, uwekezaji huu utajilipa wenyewe katika msimu wa kwanza na kusababisha kuongezeka kwa uzalishaji wa chakula cha nyumbani, haswa wakati wa kiangazi kirefu.
Mbinu bora ya kuchagua mfumo wa unyunyizaji maji ni kuchagua mfumo rahisi na bora ambao utahitaji gharama kidogo. Kuweka mfumo wa unyunyizaji maji wa gharama ya juu unahitaji ushauri wa wataalam.
Hata hivyo, kuna mifumo mingine ya unyunyizaji maji midogo ambayo inaweza kuwekwa kwa urahisi na kwa gharama nafuu, kama vile mfumo wa ndoo au bomba. Njia zingine mbadala za bei ya chini ni kama vile mfumo wa bomba la mianzi, unyunyizaji maji kwa mtungi au chupa. Wakulima wanapaswa kuwa waangalifu wakati wa kununua chombo cha kunyunyiza maji ili kuhakikisha kuwa wanapata dripu bora. Kuna aina mbili za vifaa vinavyotumika kwa kumimina maji ambavyo ni: mpira na plastiki. Dripu za mpira ni bora zaidi ikilinganishwa na za plastiki kwa sababu zinaweza kuhimili hali tofauti za hali ya hewa na zinaweza kutumika kwa hadi miaka 5.